GHARAMA YA PEMBEJEO IPUNGUZWE MSIMU WA UPANZI
Na Janelle Okongo,
Ilichapishwa Taifa leo tarehe 25/3/2022
Kilimo ni uti wa mgongo wa taifa la Kenya. Asilimia kubwa ya wananchi, imetegemea pakubwa ukulima kwa minajili ya uzalishaji bora wa vyakula ili kuzima janga la njaa. Nchi ya Kenya vilevile, inazidi kukua kiuchumi kupitia ushuru wanaotozwa wakulima kutokana na mauzo ya mazao yao.
Ni jambo la kuvunja moyo namna gharama ya pembejeo inavyozidi kupanda kila uchao. Kukodi shamba, kununua mbegu ya upanzi na madawa ya kuua wadudu kumekuwa ghali zaidi kwa mkulima kumudu. Isitoshe, matrekta ya kukokotwa na mashine ya kuvunia pia yanatozwa fedha za juu zaidi ikilinganishwa na awali. Mbolea inayostahili kuongeza rutuba kwa mashamba ili kuzidisha mazao, imegeuka kuwa kilio kwa wakulima humu nchini.
Wakulima wanahisi uzito wa kujitosa kwenye kilimo msimu huu wa upanzi. Hela zinazohitajika ili kufanikisha ukulima ni nyingi mno ikizingatiwa mna gharama ya maisha inavyozidi kupanda. Wakulima wanahofia kupata hasara ya kujihusisha na raslimali hii. Hata wakijizatiti vilivyo kuzalisha, serikali inawasaliti kwa kuagiza vyakula kutoka nchi za nje.
Serikali ichukuwe jukumu la kupunguza bei ya pembejeo na maslahi ya kifedha ya wakulima, yaangaziwe kwenye bajeti ya mwaka huu. Mazao ya wakulima watafutiwe soko nchi za nje na sio serikali kuagiza. Wakulima wanaokumbana na masaibu ya pesa ya kugharamia pembejeo, wapewe mikopo na serikali ili kurahisisha shughuli za ukulima. Kilimo ni uhai hivyo tugharamie ili kukuza taifa.
Comments
Post a Comment